Staa wa muziki wa Bongofleva Naseeb Abdul, maarufu Diamond Platnumz ametajwa kwenye orodha ya wakali wa muziki wanaowania tuzo ya BET 2021.
Diamond ametajwa kwenye kipengele cha Best International Act ambapo anachuana na wakali wengine kama Wizkid na Burna Boy wa Nigeria, Emicida wa Brazil, Headie wa UK, Aya Nakamura wa Ufaransa, Youssoupha wa Ufaransa na Young T & Bugsey wa UK.
Majina hayo yametangazwa jana Mei 27, 2021 na tuzo hizo zinataraji kutolewa Juni 28, 2021.
Hii ni mara ya tatu kwa Diamond kuchanguliwa kuwania tuzo hizo na kwani mwaka 2014 Diamond alitajwa kwa mara ya kwanza kuwania tuzo hizo na kuwa msanii wa kwanza Tanzania kufikia hatua hiyo ambapo aliwania kipengele cha Best International Act Africa lakini ushindi ulikuja kwenda kwa Davido wa Nigeria.
Mwaka 2016, Diamond akatajwa tena kuwania kipengele hichohicho huku washindani wake wakiwa ni Wizkid, Yemi Alade, AKA, Cassper Nyovest na Black Koffie ambaye ndiye alitangazwa kuwa mshindi.
Baada ya kutochaguliwa kuwania BET 2017, Diamond akizungumza katika kipindi cha XXL cha Clouds FM, Juni 21, 2017 alisema lazima mwaka 2018 atachaguliwa kwani 2017 alishindwa kwa kuwa alikuwa na kazi ya kuwasimamia wasanii wa WCB Wasafi hivyo hakufanya nyimbo nyingi kubwa.
Licha ya matumaini hayo makubwa Diamond alijikuta akizikosa tuzo hizo mwaka 2018 na miaka iliyofuatia hadi mwaka 2021 alipotajwa tena.
Ikiwa atanyakua tuzo hiyo Diamond atakuwa msanii wa pili Tanzania kufanya hivyo baada ya Rayvanny ambaye alishinda Juni 25, 2017 katika kipengele cha ‘Viewer’s Choice Best New International Act’ baada ya kuwabwaga wasanii kama Dave, Amanda Black, Changmo, Daniel Caesar, Remi na Skip Marley.
Tuzo za BET zilianzishwa mwaka 2001 na huandaliwa na kituo cha Televisheni cha Black Entertainment kwa lengo la kusherehekea mafanikio ya kazi za Wamarekani weusi katika sanaa ya muziki, uigizaji pamoja na michezo mengineyo hasa upande burudani.