Diamond Platinumz amewataka wasanii wa Tanzania kuwa wamoja wanapokuwa wanaiwakilisha nchi kwenye anga za kimataifa, na kwamba ushindani wa ndani ya nchi usiwe chanzo cha kuwagawa.
Akizungumza hivi karibuni na Wasafi Media, mkali huyo wa Baikoko ambaye ametajwa kuwania tuzo ya BET, amesema kuwa alianzisha kampeni ya ‘Swahili Nation’ kwa lengo la kuwaunganisha wasanii wote wanaotumia lugha ya Kiswahili.
“Unajua ifike sehemu sisi kama ‘Waswahili’ tuwe na kitu chetu, tuungane. Najua kila mtu ana lebo yake, kila mtu ana kampuni yake, kila mtu ana wasanii wake na vitu mbalimbali vya kutafuta riziki. Lakini kitu ambacho kitatuunganisha sisi ni kimoja, mwisho wa siku sisi sote ni Waswahili,” amesema Diamond.
Ameongeza kuwa wakati msanii mmoja ‘Mswahili’ anapoingia kwenye kuwania tuzo za kimataifa na masuala mengine, ni lazima aungwe mkono na wasanii wanaowakilisha lugha hiyo, kwakuwa anaposhinda inakuwa wameshinda ‘waswahili’.
Akitoa mfano wa jinsi anavyoweza kujitoa kuwaunga mkono wasanii ‘Waswahili’ bila kujali ushindani wao wa ndani, alimtaja Ali Kiba na Ben Po kama mfano, akieleza kuwa wakizinguliwa naye atawazingua waliowazingua.
“Wa-nigeria wao wanakwambia ‘omo naija’, Walatino wao wanakwambia ‘Latino Gang’. Na sisi Waswahili nikawaza lazima tuwe na kitu chetu ambacho kitatuweka pamoja. Ikifika hatua kama unataka kumzingua Ali Kiba nitakuzingua na mimi… ukimzingua Ben Po na mimi nitakuzingua,” amesema Diamond.
“Kwa sababu yeye mswahili na mimi mswahili. Kutakuwa na kazi za kimuziki lakini tuna cha kwetu pia kama Waswahili, ndio wanavyofanya wenzetu,” ameongeza.
Diamond anawania tuzo za BET mwaka huu katika kipengele cha International Act. Hata hivyo, kumekuwa na vutankuvute kati ya mashabiki wanaomuunga mkono kutoka Tanzania na wale walionzisha harakati kwenye mtandao wa Twitter kuhakikisha anaikosa tuzo hiyo.