Klabu ya Atletico Madrid imethibitisha meneja wao Diego Simeone amepima na kukutwa na maambukizi ya virusi vya Corona.
Wachezaji wa Atletico Madrid na benchi la ufundi walifanyiwa vipimo vya COVID-19 mwishoni mwa juma lililopita, baada ya kurejea kutoka Los Angeles, Marekani walipokuwa wakijiandaa na msimu mpya wa Ligi ya Hispania (La Liga).
“Baada ya kuchunguza sampuli hizi ndani ya maabara iligundulika kuwa mwalimu wetu Diego Pablo Simeone, amepata maambukizi ya COVID-19,” Imeeleza taarifa ya Atletico Madrid.
“Bahati nzuri meneja wetu hakuonesha dalili zozote, na kwa sasa yupo nyumbani kwa ajili ya kufuata utaratibu uliowekwa na mamlaka za afya ili kuepuka usambazaji wa virusi.”
Kutokana na majibu ya vipimo kuonyesha Simeone ameathirika, meneja huyo kutoka nchini Argentina atalazimika kujitenga ingawa hakuonesha dalili zozote kama ana maambukizi.
Kikosi cha Atletico Madrid kinatarajia kusafiri mpaka Cadiz kwa mchezo wa kirafiki kesho Jumanne, kabla hakijaanza Mshike Mshike wa La Liga Septemba 27, ambapo watanza dhidi ya Granada.