TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imefungua dirisha la kwanza la udahili kwa wanafunzi wa elimu ya juu shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2022/ 2023 litakalo anza hii leo Julai 8, 2022 hadi Agosti 5, 2022.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa ameyasema hayo hii leo Julai 8, 2022 na kudai kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita.

“Udahili wa kujiunga na shahada ya kwanza utahusu waombaji waliohitimu wa kidato cha sita wenye Stashahada na waliomaliza programu ya Foundation ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),” amesema.

Katibu Mtendaji wa Tume ya vyuo Vikuu nchini (TCU), Profesa Charles Kihampa akizungumzia kufunguliwa kwa dirisha la kwanza la udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2022/2023.

Akizungumzia sifa stahiki za kujiunga na Chuo Kikuu, Prof. Kihampa amesema waombaji wanatakiwa kusoma vigezo vilivyopo kwenye vitabu vya muongozo vya TCU, huku akiwataka kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo wamevichagua kwa maelezo ya chuo husika.

Hata hivyo, amewapa tahadhari waombaji wote wa shahada ya kwanza kuwa endapo watahitaji kupata ufafanuzi wa suala lolote juu ya udahili kuwasiliana moja kwa moja na vyuo husika ama TCU.

“Tunawaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini” ametoa angalizo Prof. Kihampa.

Amesema, waombaji wanapaswa kuzingatia mambo muhimu ikiwemo kusoma muongozo wa udahili na kuuelewa, kuingia kwenye tovuti za vyuo ili kujua taratibu za kutuma maombi, kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielektoniki na kuwasiliana na vyuo ili kupata taarifa.

Aidha, Kihampa amewataka wanachuo na wananchi kuhudhuria maonyesho ya 17 ya Vyuo vya Elimu ya Juu na Sayansi na Teknolojia, yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Julai 18 hadi Julai 23, 2022.

Majaliwa: Ruangwa tumewawezesha mkuze mtaji
Kiongozi CCM afariki ghalfa Msikitini