Waziri wa Afya. Jinsia, wazee na watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka jamii kushiriki na kufuatilia kikamilifu matatizo mbalimbali yanayowakumba Watoto.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo Wilayani Tarime Mkoani Mara alipotembelea kituo cha Nyumba Salama cha Masanga kinachotumika kulea Watoto waliokumbwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na walio katika hatari ya kukumbwa na vitendo hivyo.
“Jamii lazima ishiriki kikamilifu kufuatilia matatizo yanayowakumba wanajamii husika kama wanashindwa kufanya hivyo wanakuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo” amesema Dkt. Gwajima.
Aidha amesema kuwa katika baadhi ya maeneo nchini watoto wanafanyiwa vitendo vya kikatili na kukoseshwa haki ya elimu ilhali watumishi wanaopaswa kuingilia kati suala hilo wanabaki kimya na kuongeza kuwa baadhi ya watendaji katika ngazi mbalimbali wanabweteka na kulipwa mshahara bila kuufanyia kazi.
Awali akisoma taarifa ya Kituo cha Masanga kwa Waziri, Meneja wa Mradi wa kupinga Ukeketaji Kituoni hapo, Valerian Mgani amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya bweni, chombo cha usafiri na watoto wa kike kukatishwa masomo, kukeketwa na kuozeshwa katika umri mdogo.
Ameongeza kuwa Kituo cha Nyumba salama cha Masanga kilianzishwa na mwaka 2006 na kusajili mwaka 2015 kwa lengo la kuwahudumia watoto wahanga wa ukatili ukiwemo ukeketaji ambapo hadi sasa kituo hicho kinahudumia walengwa 34 kati yao mmoja wa kiume.
Amefafanua kuwa vitendo vya ukeketaji vinaweza kukomeshwa endapo wanaume watakaa katika makundi yao na kujadiliana jinsi ya kukomesha vitendo hivyo na kuongeza kuwa ukeketaji unaendelea kwa sababu wanaume hawajaamua kusema ukeketaji basi.