Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango, kesho Julai 23, 2021 anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Mtwara.
Akiwa mkoani humo anatarajiwa kushiriki misa ya kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha hayati Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa katika Kijiji cha Lupaso Wilaya ya Masasi.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango atazindua stendi ya mabasi Wilaya ya Nanyumbu pamoja na soko la kisasa la matunda na mbogamboga la Jidah wilayani Masasi, kuzindua kiwanda cha kubangua korosho Wilaya ya Newala pamoja na kuzungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali atakayotembelea.
Aidha, Makamu wa Rais anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Kanda ya kusini iliopo Wilaya ya Mtwara na baadaye kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya sabasaba Mtwara mjini.