Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa deni la Taifa ni himilivu kwa vipimo vya kimataifa, kwa muda mfupi, wa kati na mrefu.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo leo wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.
Amesema kuwa deni la Tanzania kwa uwiano wa pato la Taifa ni asilimia 31, wakati ukomo wa kidunia ni asilimia 55. Hivyo, bado nchi iko katika kiwango kizuri cha kuendelea kukopa kwa sababu zenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha, Waziri huyo wa Fedha na Mipango aliwaondoa hofu wale wanaodhani kuwa mikopo hupewa mtu asiye na kitu.
“Watu wengine wakisikia mkopo wanaogopo, kumbe mkopo sio msaada, anapewa mwenye chanzo cha kulipa. Masikini ambaye hana kitu kabisa hapewi mkopo. Kwahiyo mkopo ni biashara, tajiri na tajiri wanafanya biashara ya kutumia fedha,” alisema.
“Kwa maana hiyo, tutaendelea kukopa ili tutekeleze miradi mikubwa kwa uharaka. Ukitekeleza mradi mkubwa kwa muda mrefu, yaani kama ni mradi wa miaka mitano wewe ukusanye ndani ndio utekeleze kwa miaka 20, watekelezaji watakuwa wanakukwepa,” aliongeza.
Alisisitiza kuwa wataalam wote wa fedha na taasisi zote za kifedha duniani zinaiweka Tanzania kwenye kiwango bora cha kuendelea kukopa.
Vilevile, Dkt. Nchemba alitumia wakati huo kupinga hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Cham Cha NCCR – Mageuzi, Mbatia kuwa katika kipindi cha miezi tisa, Serikali ya Awamu ya Sita imekopa takribani Sh. 10 trilioni.
“Niwahakikishie watanzania, mimi ndiye natunza hizi kumbukumbu… Mheshimiwa Rais, mkopo wako wa kwanza ni huu wa sh. 1.3 trilioni ambao pia hauna riba. Na mikopo mingine ambayo tumeshasaini ni ile ya Benki ya Dunia ambayo pia ni ya masharti nafuu,” alisema Dkt. Nchemba.
Alisema ipo mikopo inayoendelea kupokelewa ambayo ilisainiwa kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mchumi huyo alieleza kuwa hakuna siku Mtanzania atagongewa hodi kudaiwa fedha zilizokopwa na Serikali, kwa sababu mkopo wa Serikali ni suala la kitaasisi na sio deni la familia moja-moja.
Hivi karibuni, kuliibuka mjadala kuhusu uhimilivu wa deni la Taifa, kukiwa na pande mbili za waliokuwa wanaunga mkono kuendelea kukopa nje ya nchi na wale waliodai mikopo hiyo sio afya kwa Taifa.