Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza jinsi ambavyo fedha zilizokusanywa kupitia tozo za miamala ya simu zilivyotumika.

Akizungumza leo, Ikulu alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, Dkt. Nchemba amesema kiasi kikubwa cha fedha zilizokusanywa kuanzia Julai hadi Novemba 2021, zilipelekwa katika mfuko wa mikopo ya elimu ya juu.

Alisema kuwa katika kipindi hicho, jumla ya Sh. 161.598 bilioni zilikusanywa, na kwamba kati ya hizo Sh. 91.66 bilioni zilielekezwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu waliokosa mikopo mwaka jana.

“Kwa zile zilizokusanywa Tanzania Bara, Shilingi Bilioni 91.66 zilikwenda kwa ajili ya mikopo ya juu kwa wanafunzi waliokosa mikopo mwaka jana,” alisema Dkt. Nchemba.

Alimshukuru Rais Samia kwa kuelekeza fedha hizo kupelekwa katika kuwasaidia wanafunzi waliokosa mikopo kuendelea na masomo yao, na kwamba kama fedha hizo zisingepatikana wanafunzi hao wangelazimika kutoendelea na masomo mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchemba amesema kuwa Sh. 1.3 trilioni za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, zilipatikana kwa njia ya mkopo usio na riba na zitalipwa kwa muda mrefu.

Alieleza kuwa fedha hizo zimetekeleza miradi mingi itakayogusa na kubadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya watanzania kwa namna ambayo haijawahi kutokea nchini.

Pamoja na mambo mengine, katika sekta ya afya, Dkt. Nchemba alisema jumla ya zabuni 245 zinatarajiwa kutekelezwa.

Waziri wa Fedha asema deni la Taifa ni himilivu
China yawafungia ndani watu milioni 1.2 baada ya watatu kupata UVIKO-19