Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dkt. John Pima na wenzake wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na kesi mbili za uhujumu uchumi zenye makosa nane.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Bittony Mwakisu washtakiwa Dkt. Pima, aliyekuwa mchumi wa Jiji Inocent Maduhu, wachumi Nuru Ginana na Alex Daniel hii leo hii leo Juni 17, 2022 wamepandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka nane kwa kesi mbili tofauti za uhujumu uchumi.
Mbali na washitakiwa hao wanne, mshitakiwa mwingine ni Mariam Mshana ambaye alikuwa Mweka hazina wa Jiji hilo ambaye hakuwepo mahakamani hapo, ambapo upande wa Jamhuri umeiomba mahakama kutoa hati ya wito na kukamatwa kwa mshitakiwa huyo ambaye ni wa pili katika kesi zote.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri umewakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Aksa Mhando na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Hamidu Simbano huku Dkt. Pima na Maduhu wakiwakilishwa na Wakili Valentine Nyalu.
Katika kesi ya kwanza inayowakabili Dkt. Pima, Mariam, Maduhu na Ginana wanakabiliwa na mashitaka manne ambayo ni ufujaji na ubadhirifu, huku makosa mengine yakiwa ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Hata hivyo, washitakiwa hao wataendelea kukaa Mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ambapo kila mmoja anapaswa kuwa na wadhamini wawili watakaoweka Sh32 milioni au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Awali, Mei 24, 2022 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwasimamisha kazi maafisa sita wa Jiji hilo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za jiji na tuhuma za kughushi nyaraka baada malalamiko yaliyotolewa na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo katika kikao cha watumishi wa jiji kilichokuwa kinaongozwa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa.
Kufuatia tuhuma hizo zilizotolewa na mbunge huyo, Waziri Mkuu aliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru kufuatilia suala hilo na kesi hizo zimeahirishwa hadi Julai Mosi mwaka huu kwa watuhumiwa kusomewa maelezo ya awali.