Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Benki ya CRDB PLC, wamesaini hati ya makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Ughaibuni ‘Diaspora Digital Hub’.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB PLC, Abdul Majid Nsekela katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Balozi Sokoine amesema mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Serikali kuwatambua, kuwasajili na kuwawezesha Watanzania wanaoishi ughaibuni kupata huduma mbalimbali na kushiriki kidigitali katika shughuli za maendeleo, biashara, uchumi na uwekezaji.

“Mfumo huu utafungua uwezekano wa fursa zaidi za ushirikiano kati ya Wizara na Benki ya CRDB, katika kazi ya uendelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya Balozi za Tanzania nje ya nchi,” amesema Balozi Sokoine.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB PLC, Abdul Majid Nsekela amesema CRDB inaamini kuwa kuanza kwa mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora utakuwa na manufaa kwa Serikali na Benki ya CRDB.

“Kwa ujumla mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora utasaidia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kusaidia kufahamu idadi ya Diaspora walioko ulimwenguni na kutunza taarifa za watanzania walioko nje,” amesema Nsekela.

Aidha. ameongeza kuwa Diaspora Digital Hub pia itasaidia kupata taarifa za fursa za uwekezaji nchini na kuwatambua wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini, kuisaidia Serikali katika zoezi la sensa litakalo fanyika mwezi Agosti, 2022, kusaidia kupata taarifa sahihi za pamoja na kuisaidia Wizara kupanga bajeti yake.

“CRDB inaahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub unakamilika kwa wakati.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akizungumza katika hafla hiyo amesema Mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub utakapokamilika utaiwezesha Serikali kuwa na kanzidata ya uhakika kuhusu Diaspora kote ulimwenguni.

Dkt. Pima na wenzake kizimbani kwa uhujumu uchumi
Mzozo wa Rwanda na DRC wazidi kufukuta