MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema kuna umuhimu wa nchi hiyo kufikiria kuunda chombo rasmi kitakachopewa jukumu la kisheria kusimamia, kuangalia na kupima utekelezaji wa mambo yote yanayohusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Othman ameyasema hayo hii leo Juni 17, 2022 ofisini kwake mjini Zanzibar, wakati wa maongezi yake na Balozi mdogo wa Uingereza nchini Tanzania Rick Shearn, aliyetaka kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya uimarishaji wa demokrasia na serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Amesema, kuwepo kwa chombo hicho kutasaidia kuziona changamoto na kupanga kwa pamoja namna bora ya kuzipatia ufumbuzi ili serikali hiyo iweze kuendelea na kuwa na manufaa kwa Wazanzibar.

“Jambo hili ni miongoni mwa mapendekezo kadhaa yaliyowasilishwa serikalini kwa ajili ya kujadiliwa ili yatakapokubalika hatua rasmi za kuundwa kwa chombo cha aina hiyo ziweze kuchukuliwa,” amefafanua Makamu huyo.

Aidha, katika kuendeleza suala hilo amesema ipo haja ya kuitishwa kwa makongamano ya Kitaifa ili kupata maoni na fikra mbali mbali za wananchi katika kuweka mkakati bora wa serikali hiyo.

“Yapo masuala mengi yanayoainishwa kwa nia ya kuyafanyia mageuzi makubwa ikiwemo tume ya Uchaguzi kwa kuwa matumaini ya wananchi ni kuwepo mabadiliko ya kweli katika masuala mbali mbali hasa mambo yanayohusu uchaguzi,” amesema.

Amezidi kufahamisha kuwa, kutokana na kukosekana utulivu wa kisiasa, Zanzibar imepoteza mambo mengi ikiwemo misaada ya maendeleo na kusisitiza kwamba wananchi hawana budi kuwa wavumilivu wakati viongozi wakiendelea na juhudi za kujenga mustakabali mwema wa nchi yao.

Naye Balozi mdogo wa Uingereza nchini Tanzania, Rick Shearn amesema shughuli za maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji zinahitaji hali bora, utulivu na mazingira mazuri ya kisiasa na kwamba kuwepo serikali ya Umoja wa Kitaifa kutasaidia kuleta utulivu Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Akizungumzia tatizo la dawa za kulevya, Balozi huyo amesema nchi yake itaendelea kuisaidia Zanzibar kuwajengea uwezo watendaj wa Mamlaka ya Kupambana na kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar ili zoezi hilo liweze kufanikiwa.

Ukraine yalalamikia uharibifu wa makombora ya Urusi
WHO yathibitisha uhaba wa chakula Sudan