Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Franklin Rwezimula amesema kuwa katika mabadiliko ya sera mpya ya elimu, mafunzo na mitaala, kutakuwa na somo jipya la Sayansi ya Kompyuta litakalowasaidia wanafunzi kuwa wataalam wabunifu na wadadisi kwenye eneo hilo, na kuwawezesha kuzitengeneza.
Dkt. Rwezimula ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya walimu yenye lengo la kuwapatia mbinu mpya za matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na vishkwambi katika kufundishia ili nao wakafundishe wenzao.
Aidha amesema kuwa tayari rasimu za mapitio ya Sera ya Elimu, Mafunzo na ile ya Mitaala zimekamilika na wakati wowote itatolewa kwa wadau ili waone kilichopendekezwa na kutoa maoni yao mengine ya mwisho.
Amebainisha kuwa lengo la kufanya mapitio na mabadiliko hayo ni kutekeleza ahadi aliyotoa Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya mapitio ya sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala ili kuwezesha kutoa elimu ujuzi, lakini pi akuwa na sera na mitaala inayoakisi mahitaji ya sasa na baadae .
“Katika kuzingatia maono ya Rais wetu, kwenye mabadiliko hayo toleo hilo la elimu la mwaka 2023 tutakuja na somo linaitwa ‘Kompyuta Sayansi’ ambalo litasaidia wanafunzi kubuni na kudadisi mambo ya kompyuta na kuzitengeneza ambapo tunaamini litakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Alisema kuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa kufundisha somo hilo, wameanza kutoa mafunzo kwa walimu wa Tehama namna ya kutumia vishkwambi katika kufundishia ili nao wakafundishe wenzao.
Dunia imezama kwenye Sayansi na Teknolojia, hivyo Wizara inaegemea kuwanoa walimu hao na kwamba wazitumie tena ‘analogi’ bali waendane na mabadiliko hayo, na kwamba wanatakiwa kubeba dhamana ya kwenda kuwasaidia wenzao.
“Mafunzo haya yako chini ya mradi wa miaka mitano unaolenga ‘kuboresha mazingira ya ujifunzaji, ufundishaji kwenye shule zetu za sekondari (SEQUIP), ikiwa ni utekelezaji wa mapinduzi makubwa ya elimu”
kwa upande wake mratibu wa SEQUIP, Dk Mollel Meigaru alisema kuwa mafunzo hayo yanayolenga kuimarisha elimu ya sekondari nchi nzima, yako chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) kwa mkopo wa dola milioni 500.
Mafunzo hayo yamekuja ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu aliyoyatoa siku ya Mei mosi 2023 baada ya kusoma moja ya bango la walimu walioomba kupatiwa mafunzo ya jinsi ya kutumia vishkwambi kufundishia.
“Mbali na mafunzo haya, pia mradi umewafikia walimu 18,000 kwa kuwapa nyenzo za namna bora ya kufundisha masomo ya sayansi, na kuhusisha na tehama, lakini pia unalenga kujenga miundombinu kwa shule za sekondari zikiwemo 1000 za mchanganyiko na zingine 26 za wasichana.