Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amewataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuahidi kushirikiana na watumishi wote katika kutekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi ili kufikia matarajio ya Serikali.
 
Dkt. Tax ametoa rai na ahadi hiyo katika Ofisi za Wizara zilizpo katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma hii leo Oktoba 7, 2022 baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.
 
Amesema, “Sisi ni timu ya ushindi, endeleeni kuchapa kazi, nitashirikiana na watumishi wote wa Wizara, kuhakiksiha tunatekeleza majukumu yetu kwa viwango na kwa muda sahihi, muwe wabunifu na tujitahidi kufanya kazi kama timu ili kufikia matarajio ya Serikali yetu na wananchi wote kwa ujumla. “

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax (kulia) akiwa na Balozi Liberata Mulamula katika makabidhiano ya ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dodoma hii leo Oktoba 7, 2022.

Aidha ameongeza kuwa, kazi ya kukuza uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali, Jumuiya za kikanda na kimataifa haiwezi kufanikiwa ikiwa watumishi hawatashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kama timu na kusisitiza kuzingatia weledi, uzalendo na ubunifu kwa maslahi mapana ya taifa.
 
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Balozi Liberata Mulamula amewashukuru Watumishi wa Wizara kwa ushirikiano waliompatia alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambao ulimuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
 
Amesema, “Nimeacha timu imara wote wanaume kwa wanawake, nawashukuruni sana kwa ushirikiano mlionipatia na niwaombe muendelee na moyo huo huo ili muendelee kufanikisha majukumu ya Wizara.”

Awali, akizungumza katika hafla hiyo Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbrouk Nassor Mbarouk amemshukuru Balozi Mulamula kwa ushirikiano aliompatia katika kipindi chake na kumsihi aendelee kushirikiana nao kwa kuzingatia hazina kubwa ya uzoefu na ujuzi alionao katika sekta ya mambo ya nje.
 
Akiwakaribisha katika hafla hiyo ya makabidhiano Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amesema, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kumuahidi Dkt. Tax ushirikiano na kwamba watumishi wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuzingatia sheria, taratibu na kanuni.

Afrika kinara watu kujiuwa, uelewa chanzo kikuu
Idadi wagonjwa wa afya ya akili yaogofya