Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amewashukia baadhi ya wabunge baada ya kusikia kelele wakati wa kuwasilisha taarifa ya shughuli ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Dkt. Tulia alifikia uamuzi huo baada ya kusikia sauti za juu muda mfupi baada ya wabunge kusimama kwa muda kwa maelekezo yake na kukaa kimya kumkumbuka Hayati Dkt. Magufuli.
“Waheshimiwa wabunge kelele zinatoka wapi, naona hatuko pamoja, nazisikia kelele katika jambo hili zito lililoikumba nchi yetu,” amesema Dkt. Tulia.
Hayati Dkt. Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021, shughuli za mazishi yake kama alivyoeleza Dkt. Tulia bungeni zilifanyika kwa kupitia mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Geita na Visiwa vya Zanzibar. Hayati Magufuli alizikwa Machi 26, 2021 nyumbani kwao Chato mkoani Geita.
Mkutano wa Tatu wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeanza leo jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine utajadili na kupitisha bajeti za wizara mbalimbali pamoja na Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021.