Mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Donald Ngoma huenda akawa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu, kutokana na matatizo ya kiafya yanayomkabili katika kipindi hiki ambacho Young Africans inahitaji kurejesha makali yake kwenye michezo ya ligi kuu ya soka Tanzania bara.
Ngoma hakumaliza mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita, ambapo mabingwa hao watetezi walicheza dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, na kutoka sare ya bila kufungana.
Afisa Habari wa Young Africans, Dismas Ten amethibitisha juu ya taarifa hizo kwa kusema wanasubiri ripoti ya kitabibu juu ya mchezaji huyo, kwa kuwa alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.
Akizungumza juu ya afya ya Ngoma, Ten alisema: “Ni kweli Ngoma ana tatizo la afya na tunasubiri ripoti ndani ya saa 24 hadi 48 kutoka kwa daktari kujua maumivu ya jeraha yake, baada ya hapo tutatoa ripoti.”
Ikumbukwe kuwa, hadi sasa Young Africans inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, licha ya kuzidiwa pointi mbili dhidi ya Simba ambao wanaongoza msimamo wa ligi hiyo.
Ikiwa Ngoma atakuwa nje na kukosa michezo kadhaa kuna uwezekano likawa pigo kwa Young Africans, kwa kuwa mshambuliaji huyo ni muhimu katika kikosi cha kwanza.