Beki mpya wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Mamadou Doumbia amewaahidi makubwa Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo kwa kusema amekuja kufanya kazi na sio maneno maneno.
Doumbia aliwasili jijini Dar es salaam Jumamosi (Januari 21), baada ya kukamilisha taratibu wa kujiunga na Young Africans akitoke Stade Malien ya nchini kwao Mali.
Beki huyo ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Mali kinachoshiriki Fainali za Mataifa Bingwa barani Afrika ‘CHAN’ mwaka huu 2023, amesema amefurahi kusajiliwa Young Africans ambayo inafuatiliwa sana na Mashabiki wa soka nchini kwao.
Amesema anaijua klabu hiyo kutokana na kuwa na uimara wa kupambana uwanjani, huku ikisheheni wachezaji wenye vipaji ambao wanachagiza ushindani wa kuingia kwenye kikosi cha kwanza.
“Kwanza kabisa nimefurahi sana kufika hapa, Young Africans ni klabu kubwa sana kule nyumbani kwetu Mali, kwani ni timu inayofuatiliwa ma watu wengi, hivyo kuja hapa ni jambo kubwa sana kwangu kama mchezaji.”
“Mimi sio mtu wa maneno sana, kazi yangu ni uwanjani na Mashabiki wategemee mazuri kutoka kwangu. Nawapenda sana.”
“Nafahamu hapa Young Africans kuna ushindani mkubwa, lakini nitajitahidi kupambana kuingia katika kikosi cha kwanza, licha ya kuwakuta mabeki wengine ambao wanafanya vizuri.” amesema Doumbia
Beki huyo mwenye umri wa miaka 27, huenda akawa sehemu ya kikosi cha Young Africans kitakachoshuka dimbani baadae leo Jumatatu (Januari 23), kuikabili Ruvu Shooting Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.