Katibu Mkuu wa Kinga na Tiba kwa wana Michezo Tanzania na Daktari Mkuu Mwandamizi Yanga Afrika Dr Nassoro Ally Matuzya, amefunguka na kuweka hadharani matatizo yanayomuandama kiungo wa mabingwa wa soka Tanzania bara Thaban Scara Kamusoko, ambaye hajaonekana uwanjani kwa kipindi kirefu.

Matuzya amefunguka kupitia mitandao ya kijamii kwa kuandika ujumbe ambao umeainisha tatizo la kiungo huyo kutoka nchini Zimbabwe, sambamba na utaratibu wa matibabu ambao kama utafuatwa huenda akapona na kurejea uwanjani kwa wakati.

Ufuatao ni ujumbe wa Dr Nassoro Ally Matuzya aliounadika kwenye mitandao ya kijamii.

WAZO NA USHAURI

Mimi Dr Nassoro Ally Matuzya Katibu Mkuu wa Kinga na Tiba kwa wana Michezo Tanzania na Daktari Mkuu Mwandamizi Yanga Afrika, nimepitia na kudurusu Matatizo ya Mchezaji THABAN SCARA KAMUSOKO nikiwa na jopo la Madaktari wa fani ya Mionzi na Viungo vya Binadamu tukiwa na mchezaji na tumebaini kuwa Mchezaji THABAN SCARA KAMUSOKO bado anasumbuliwa na Goti lake la kushoto aliloumia katika Mechi kati ya Yanga Vs Lipuli uliofanyika Uwanja wa Uhuru ambapo aliumia goti hilo na kutoka baadae.

Amekuwa akijitibu bila mafanikio na Jana 27/11/2017 alijisalimisha kwenye jopo la Madaktari tajwa hapo juu ambao tulimchunguza kwa kina na kubaini kuwa ana tatizo la kupasuka kwa kikombe cha ndani cha mguu wa kushoto ambacho kinaelekea kupata nafuu baada ya Matibabu ambayo hayakuwa na mpangilio unaoeleweka.

Kwa maana hiyo Jopo la Madaktari hao tulikubaliana nao kuanza kumtibu KAMUSOKO tukianza kwa vipimo na Dawa ambazo zinagharimu kiasi kisichopungua Tsh 720,000/- kwa Mchanganuo ufuatao:-

  1. Kipimo cha MRI 480,000/-
  2. Dawa na Vifaa tiba za kuanzia ni Tsh 158,000/-
  3. Vipimo vingine vya X Ray, Ultra Sonic Sound na Kumuona Daktari Tsh 82,000/-

Kimsingi jopo la Madaktari hawa wamekubaliana kumsaidia Mchezaji huyu kwa Moyo baada ya yeye kubainisha Ari ya kutaka kurudi uwanjani kuisaidia timu yake.

Kwa heshima na Upendo Mkubwa naomba kuwashirikisha wadau wote wa Yanga kuona ni njia ipi sahihi ya kumsaidia Mchezaji wetu ili Jopo la Madaktari hawa liendelee Kumsaidia endapo kiasi hicho kitapatikana. Ni vyema tukasema ni namba gani itumike pia Aidha ya Mchezaji au za Maadmin au Uongozi wa Klabu

Naomba kuwasilisha.

Dr Nassoro Ally Matuzya

Mratibu Afya – Yanga

Majaliwa atoa onyo kwa watumishi
Wachezaji TP Mazembe wajazwa noti