Mshambuliaji kutoka nchini Ivory Coast, Didier Drogba amefanya maamuzi ya kwenda kucheza soka nchini Marekani katika ligi ya MLS, baada ya kukubali kusaini mkataba wa kuitumikia klabu ya Montreal Impact.

Maamuzi ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 37 ya kuelekea nchini humo yanadhihirisha soka lake litafikia kikomo katika ligi ya MLS baada ya kucheza kwa kipindi kirefu katika baadhi ya ligi za barani Ulaya.

Drogba msimu uliopita alirejea nchini England baada ya kusajiliwa na klabu ya Chelsea akitokea Galatasaray ya nchini Uturuki.

Kabla ya kufanya maamuzi ya kujitia kitanzi cha kuitumikia Montreal, mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast, alikua katika mipango ya kutaka kujiunga na klabu ya Chicago Fire ambayo pia inashiriki ligi ya MLS.

Rais wa klabu ya Montreal, Joey Saputo amepasua ukweli wa kufanikisha mipango ya kubadili mawazo ya mshambuliaji huyo kwa kusema walitumia mbinu mbadala kumpata Drogba ambaye huenda angejiunga na timu pinzani.
Amesema ni wakati mzuri kwao kuwa katika hali ya kujiamini kipindi chote kutokana na azma walihoikamilisha ya kuwa na mshambuliaji mwenye hadhi kubwa duniani kote.

Drogba alianza kuwika katika soka la barani Ulaya akiwa na klabu ya Olympique de Marseille kati ya mwaka 2003–2004 na kisha alijiunga na Chelsea kuanzia mwaka 2004 – 2012.

Alielekea nchii China baada ya kusajiliwa na Shanghai Shenhua ambayo aliitumikia kwa mwaka mmoja kisha mwaka 2013 alielekea nchini Uturuki kujiunga na klabu ya Galatasaray kabla ya kurejea tena Chelsea kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Lowassa Ashindilia Msumari Wa Richmond Baada Ya kuingia Chadema
Bayern Munich Washtukia Mchezo Wa Man City