Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich wanajipanga kufanya mazungumzo na Pep Guardiola, ili kukamilisha azma ya kumsainisha mkataba mpya wa kuendelea kukinoa kikosi cha klabu hiyo kwa miaka mingine ijayo.

Mwenyekiti wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Munich, Karl-Heinz Rummenigge amethibitisha kufanyika kwa mipango ya kumsainisha mkataba mpya meneja huyo kutoka nchini Hispania na ana uhakika itakamilika.

Mkataba wa sasa wa Guardiola, unatafikia kikomo mwishoni mwa msimu ujao wa ligi, hali ambayo inazusha hofu miongoni mwa viongozi wa FC Bayern Munich kwa kuhisi huenda klabu nyingine duniani zikaanza kumnyatia.

Juma lililopita Rummenigge, alizungumza na kituo cha televisheni cha BeIN Sports na kueleza kwa uchache juu ya mipango hiyo, lakini hakutaka kuweka wazi ni vipi walivyojipanga kwa ajili ya kumshawishi Guardiola ili akubali kusaini mkataba mpya.

Klabu ya Man city ya nchini England, imekua ikitajwa sana kumuwania meneja huyo, hali ambayo inahisiwa huenda imekua msukumo kwa viongozi wa Bayern Munich kuanza mapema mchakato wa kutaka kumsainisha mkataba mpya.

Hata hivyo Pep Guardiola aliwahi kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza wazi mustakabali wake ndani ya FC Bayernm Munich na alisema ana matarajio ya kupanga mbivu na mbichi ndani ya mwaka huu.

Guardiola alipokea kijiti cha umeneja klabuni hapo kutoka kwa Jupp Heynckes, na amekua na mafanikio makubwa tangu alipokubali kufanya kazi na klabu hiyo mwaka 2013.

Drogba Atimkia Marekani
Dkt Slaa Aelezea Mkutano Wa Chadema Na Lowassa, “Lowassa Sio Mgombea Wa Chadema”