Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Eden Hazard, anapanga kustaafu kabisa kucheza mpira wa miguu ingawa ana ofa mezani kutoka Ligi Kuu ya Marekani, kwa mujibu wa ESPN.
Taarifa zinaeleza kuwa Klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada ambayo inashiriki Ligi Kuu Marekani (MLS), imedhamiria kumsajili Kiungo huyo wa zamani wa klabu za Lile, Chelsea na Real Madrid.
Hazard mapema wiki hii alifikia muafaka wa kuvunja mkataba wake na Real Madrid ya Hispania, baada ya kukumbwa na majeruhi ya mara kwa mara tangu alipotua hapo akitokea Chelsea.
Mchezaji huyo hakuwa na wakati mzuri tangu alipojiunga na vigogo hao wa Hispania, Real Madrid na hilo lilisababisha kumfanya kutokupata nafasi ya kucheza hadi kufikia hatua ya kuondoka klabuni hapo.
Hazard amevunja mkataba na Real Madrid kwa makubaliano ya pande zote mbili na hiyo inatokana na mchezaji huyo kutokuona dira ya maendeleo yake ndani ya timu hiyo.
Hivyo mchezaji huyo inaelezwa amepanga kustaafu kabisa kucheza mpira baada ya kuondoka klabuni hapo.
Hazard amekuwa mchezaji bora kwa miaka mingi haswa kipindi akiitumikia Chelsea ya England.
Lakini mambo yalibadilika alipojiunga na Real Madrid mwaka 2018 na kuanza kuandamwa na majeraha na kumfanya kupotea kabisa katika ramani ya soka.
Wengi walitarajia winga huyo ataungana na mastaa mbalimbali kwenda Uarabuni ambapo wanalipwa fedha nyingi zaidi, lakini mchezaji huyo inaelezwa ameamua kuachana na mpira wa miguu baada ya kufanikiwa kushinda kila taji katika ngazi ya klabu.