Uongozi mbovu, elimu duni ya uendeshaji wa taasisi za fedha pamoja na mikopo mibaya imetajwa kuwa kikwazo katika maendeleo ya vyama vya ushirika nchini.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Elimu na Mafunzo kutoka shirikisho la vyama vya ushirika Tanzania TFC, Floriani Haule katika mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji viongozi wa vyama vya ushirika vya Nyanda za juu kusini ikiwemo Njombe.
Amevishauri vyama vya ushirika kupunguza ukopaji wa fedha katika mabenki na badala yake vijiimarishe kupitia mitaji ya wanachama pamoja na kubuni miradi ya kuongeza uwezo wa vyama hivyo.
”Changamoto ambazo tuliweza kuzibaini katika vyama vya ushirika moja ya changamoto kubwa tuliyoibaini tukasema lazima tumzungumze ni kuhusu suala zima la vyama vya ushirika kuikimbilia mikopo pasipo wao wenyewe kufanya tathimini ya kina, ni kweli fursa pengine zimetolewa na serikali yetu hasa katika benki ya kilimo kwamba wakulima wakope na wakope kupitia vyama vya ushirika’’amesema Haule.
Aidha, amesema kuwa ni vyema vyama vya ushirika vinapokwenda kukopa viwe vimeandaliwa, viongozi na watendaji wawe wameandaliwa waone namna ya kufanya tathimini ya mahitaji ya mkopo kwamba wanahitaji kiasi gani.
Hata hivyo, ameongeza kuwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na idadi kubwa ya vyama vya ushirika vinavyo kufa baada ya kushindwa kujiendesha kuwa kumekuwa na viongozi waliokosa uzalendo ambao wamekuwa wakitumia vyama hivyo kwa maslahi binafsi.