Waziri wa mambo ya ndani nchini Kenya Kithure Kindiki amesema serikali itaubadilisha msitu wa Shakahola kuwa eneo la kumbukumbu ya Kitaifa, baada ya zaidi ya waumini 250 kufa kwa kufunga kula, wakiaminishwa kuwa watamuona MUNGU.
Hatua hiyo imetangazwa na Kindiki ambaye amesema baada ya zoezi la uokoaji wa miili iliyozikwa katika msitu huo wa ekari 800 kukamilika, eneo hilo litakuwa makumbusho ili watu wasisahau kilichotokea nchini Kenya.
Amesema, “Serikali ina ushahidi wa kutosha wa kumfungulia mashitaka kiongozi wa dhehebu hilo mtuhumiwa mkuu, Mchungaji Paul Mackenzie kwa mauaji ya kimbari baada ya kudaiwa kuwashawishi waumini wake kufunga hadi kufa ili waende mbinguni.”
Aidha ameongeza kuwa, wengi wa wahasiriwa wa tukio hilo ni wanawake na watoto ambao walikufa kwa njaa, lakini wengine walinyongwa, kupigwa, au kukosa hewa, na akaongeza kuwa tangu kuanza kwa operesheni hiyo mwezi Aprili, miili 251 imepatikana, Watu 95 kuokolewa na washukiwa 35 wamekamatwa.