Imeelezwa kuwa gharama kubwa za matibabu ikiwa ni pamoja na kumuona daktari kwa ajili ya vipimo kunachangia watu kuamua kununua dawa bila kupima na kujua tatizo kabla ya kuanza ‘dozi’.

Hayo yameelezwa na wataalamu wa afya (mafamasia), katika kipindi cha afya tips kinachorushwa mtandaoni na chombo cha habari cha mtandaoni cha Dar24 Media walipoulizwa ni nini kinasababisha watu kuamua kutumia dawa bila kupima ama kushauriwa na wataalamu wa afya.

“Watu wapunguze bei za kuona madaktari, maana unakuta kuna hospitali kubwa ukienda kumuona daktari 100,000 (Kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi laki moja), 50,000 (elfu hamsini), kwa hiyo ile inawafanya watu waogope kwenda kumuona daktari hivyo wanakuja moja kwa moja Pharmacy (Duka la dawa) bila maelekezo yoyote yale kutoka kwa daktari,” amesema John ambaye ni Famasia.

Wataalamu hao wameeleza kuwa kutumia dawa bila maelekezo ya Wataalamu wa afya kunaweza kunaweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na ini na figo kushindwa kufanya kazi.

“Ukizidisha dawa inaweza kusababisha madhara kwenye figo, kwenye maini pamoja na moyo, kuna dawa nyingine ukinywa presha inapanda, ukishapanda presha maana yake moyo wako unapiga kwa nguvu, mishipa ya damu inapasuka, kichwa na mwishowe unakufa,” ameeleza John.

“Unapokunywa dawa nyingi, inapofika kwenye damu, kabla haijafika kwenye damu inachujwa kwanza kwenye maini na figo ili kupunguza sumu, hivyo unapozidisha unaua ini pamoja na figo,” amefafanua John.

Silvanus ambaye ni Mfamasia aliyekuwepo katika kipindi icho anaeleza kuwa, “Dawa ya haraka sana ambayo watu wengi wanaitumia wakiugua kichwa ni Paracetamol/panadol lakini kitu ambacho hawajui ni kwamba panadol inaua sana kwa haraka ikitokea umezidisha kiwango, na dawa ambayo inaharibu ini kwa haraka sana.”

Wataalamu hao wameshauri Hospitali binafsi pamoja na za umma kuhakikisha wanapunguza gharama za matibabu pamoja na za kumuona daktari huku wakishauri wananchi kuhakikisha kwamba wote wanakuwa na bima za afya ili kuweza kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za afya kwa gharama nafuu.

BONYEZA KITUFE HAPA CHINI KUTAZAMA KIPINDI CHOTE

PICHA: Dkt. Mpango azuru kaburi la Magufuli
Tusherehekee kwa kiasi - RC Kunenge