Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama pamoja na Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Telesphore Mkude, wameeleza kuhusu funzo linalopaswa kuzingatiwa kufuatia ajali ya moto uliozuka baada ya roli la mafuta kuanguka katika eneo la Msamvu Mjini Morogoro, iliyosababisha vifo vya watu 75.
Wakizungumza katika mahojiano maalum na Dar24, Jumapili, Agosti 11, 2019 wakati wa zoezi la utambuzi wa miili na kuwaombea marehemu katika viwanja vya Shule ya Sekondari Morogoro, viongozi hao walisema ni muhimu jamii kuchukua tahadhari na kujiandaa kiroho wakati wote.
Waziri Mhagama alisema kuwa tukio kama hili liliwahi kutokea mkoani Mbeya na kwamba watu walipaswa kujifunza na kuyatambua mazingira hatarishi.
“Tukio lililotokea Mbeya lilikuwa ni fundisho zuri tu la kutosha kwa Watanzania, kwa tukio hili ambalo linafanana na lile la Mbeya. Kwa hiyo mafunzo yapo mengi, yale ambayo ni ya kawaida yanayojirudia na mengine mapya ambayo tunapaswa kujifunza kwayo,” Waziri Mhagama aliiambia Dar24.
Aliongeza kuwa Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wake kuhusu kuchukua tahadhari na kutambua maeneo pamoja na matukio hatarishi.
“Lakini kwetu sisi kama Serikali tunapaswa kuendelea kuelimisha Wananchi, kitu ambacho kinaendelea kufanyika; na pia kuweza kuangalia utendaji kazi wa vyombo vyetu mbalimbali katika kusimamia matukio haya ambayo yanatokea mara nyingi barabarani,” aliongeza.
Kwa upande wa Askofu Mkude, alisema kuwa tukio hilo linatoa funzo la kiroho na kuwakumbusha binadamu kuwa wakati wote wanapaswa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu.
“Tukio hili linatupa sisi funzo kwamba tumezaliwa, tumekuja hatuna kitu na tunaondoka hatuna kitu. Kumbe haya tunayojipatia katikati na kujilimbikizia kwakweli yana mwisho wake na tunafika wakati ambapo tunaondoka kama tulivyo na hatuna kitu,” Askofu Mkude aliiambia Dar24.
“Mtume Paulo anasema hata kama ni njaa, majanga, kifo, havitusumbui sana kwa sababu tunajua tumekuja hivi, tunaacha hayo lakini upendo wetu na Mungu hauwezi kutengana nasi. Kwahiyo, sisi tukumbushane kwamba… tufanye kazi zetu, tushughulikie yote, lakini chondechonde tusimsahau Mungu.
Miili ya waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ilizikwa katika makaburi ya Kola Hill Mjini Morogoro na kuongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.