Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na kusema kwa kutumia utaratibu wa kushirikisha Sekta Binafsi, unaendelea na manunuzi ya makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa Expressway kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 205 unafanyika.
Prof. Mbarawa ameyasema hayo katika hotuba yake aliyoiwasilisha Bungeni jijini Dodoma hii leo Mei 22, 20223 na kuongeza kuwa hadi sasa kazi inayoendelea ni uchambuzi (evaluation) wa Makandarasi walioonesha nia (Expression of Interest) ya kutekeleza mradi huu kwa sehemu ya kutoka Kibaha – Chalinze yenye urefu wa kilometa 78.9. Kwa sehemu ya Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 126.1.
Amesema, “kwa sehemu ya Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 126.1, Mshauri Elekezi anaendelea na kazi ya Upembuzi yakinifu, Mheshimiwa Spika, hii itakuwa ni mara ya kwanza katika
historia ya nchi yetu kuwa na mradi mkubwa hapa nchini ambao utatekelezwa kwa utaratibu wa PPP.”
Aidha, Prof. Mbarawa ameongeza kuwa pia Serikali kupitia Wizara inaendelea na ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya mradi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza (Km 1,219) uliogawanyika katika vipande vitano.
“Hadi kufikia Aprili, 2023 hatua ya utekelezaji iliyofikiwa kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (Km 300) ni asilimia 98.14; Morogoro – Makutupora (Km 422) asilimia 93.83; Mwanza – Isaka (Km 341) asilimia 31.07; Makutupora – Tabora (Km 368) asilimia 7; na Tabora – Isaka (Km 165) asilimia 2.39,” amefafanua Waziri Mbarawa.