Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inatarajia kuanza utoaji wa mafunzo maalum ya muda mfupi kwa wafugaji wa samaki, ili kukuza tasnia hiyo na kuleta tija kwa nchi na wananchi kwa ujumla, kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji – EAC TRUEFISH PROJECT.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Sekta ya Uvuvi) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohammed Sheikh, mara baada ya wizara hiyo kuingia hati ya makubaliano kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT).

Amesema, serikali imeweka msisitizo kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo uvuvi kwa kuweka fedha nyingi kwenye ukuzaji viumbe maji hususan ufugaji wa samaki, hivyo kuna haja ya kuweka mafunzo maalum katika ufugaji wa viumbe maji.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania – FETA, Dkt. Semvua Mzighani (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania – AAT, Dkt. Charles Mahika (kulia), wakibadilishana hati ya makubaliano kati ya FETA na AAT ili wafuga samaki kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na FETA kupitiaMradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji – EAC TRUEFISH PROJECT, unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa – FAO.

“Huu ni ushirikiano kati ya wizara kupitia chuo cha FETA, kwa kuwa serikali imeweka fedha nyingi katika ufugaji viumbe maji, kuwa na mafunzo ya namna hii ya ufugaji wa samaki na kutengenza mitaala inayokubalika kwa Afrika Mashariki ni suala la msingi ili kufuga kwa tija,” amesema.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania – FETA, Dkt. Semvua Mzighani amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa muda wa wiki moja hadi mbili Kampasi ya FETA iliyopo jijini Mwanza, ambapo kwasasa walengwa ni wale wa Bonde la Ziwa Victoria walioanza kufuga samaki.

Amesema, mafunzo hayo yatakuwa na mbinu mpya na aina nzuri ya ufugaji ambayo itampa faida mfugaji kwa sababu ufugaji ni biashara na kwamba wananchi ambao pia bado hawajaanza ufugaji samaki wanaruhusiwa kupata mafunzo hayo.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakuzaji Viumbe Maji Tanzania – AAT, Dkt. Charles Mahika amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao hususan katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa chakula bora cha samaki, mafunzo ya kuzalisha vifaranga bora vya samaki pamoja na upatikanaji wa masoko ya samaki.

Dante: KMC FC tunazitaka alama sita ugenini
CCM yatia mkono sakata la mgomo Kariakoo