Serikali nchini Hispania imesema itaweka hatua kali za ulinzi kwa ajili ya fainali ya UEFA siku ya Jumamosi kwa kuhofia hatari ya kiusalama.
Mamlaka za usalama nchini humo zimesema operesheni ya polisi inayojiandaa kwa ajili ya fainali kati ya Liverpool na Tottenham itakuwa kubwa ambayo haijawahi kushuhudiwa katika tukio la kandanda katika mji huo mku wa Hispania.
Taarifa kutoka nchini humo zinasema hatua hizo zitakuwa zaidi ya zilizochukuliwa katika fainali ya mwaka jana ya Kombe la Amerika Kusini Copa Libertadores kati ya mahasimu wa Argentina River Plate na Boca Juniors, mechi ambayo pia ilitajwa kuwa yenye hatari kubwa ya kiusalama.
Zaidi ya polisi 4,700 watahusishwa katika operesheni ya Champions League, ambayo kwa mara ya kwanza itajumuisha ndege zisizoruka na rubani kufuatilia mienendo ya mashabiki.
Zaidi ya mashabiki 30,000 wa England wanatarajiwa kutizama fainali hiyo katika uwanja wa Wanda Metropolitano wenye uwezo wa kuwakaribisha watu 68,000.