Shirikisho La Soka Duniani FIFA limetoa ratiba ya fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazopigwa nchini Qatar, ambapo michezo minne itachezwa kwa siku, na hatua ya fainali itafanyika wiki moja kabla ya sikukuu ya Noeli (Krismasi).
Michuano hiyo mikubwa ya soka duniani imepangwa kuanza kurindima Novemba 21, 2022 na hii itakua mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia kufanyika kipindi cha majira ya baridi kwa nchi za Ulaya.
Kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo, mashabiki watashuhudia michezo minne kwa siku, ambapo mchezo wa kwanza utakuwa saa 7 mchana, wa pili saa 10 jioni, watatu saa 1 usiku na wa nne saa 4 usiku kwa saa za Qatar, sawa na saa za Afrika Mashariki.
Michezo ya hatua ya makundi itamalizika Desemba 02, huku ile raundi ya hatua ya 16 bora itaanza kuchezwa kati ya Desemba 03 hadi 06.
Mashabiki watapata mapumziko kwa siku tatu, kabla ya kushuhudia michezo ya Robo Fainali, ambayo itaanza Desemba 09 na 10. Fainali hizo zitakuwa na mzuka wa Krismasi, ambapo hatua ya Nusu Fainali itapigwa Desemba 13 na 14. Fainali ya michuano hiyo itafanyika Doha, Desemba 18 kwenye Uwanja wa Lusail, saa 12 jioni.