Familia ya rapa Nipsey Hussle aliyeuawa kwa kupigwa risasi Machi 31 mwaka huu, imekataa michango ya kifedha ya wadau mbalimbali iliyolenga kuhakikisha watoto wake wawili hawayumbi kifedha.
Kwa mujibu wa familia hiyo, marehemu alitengeneza misingi imara ya kifedha kwa ajili ya wanaye, Emani (7) na Kross, (2) ili wasipate shida endapo hatakuwepo.
Kulikuwa na juhudi mbalimbali za wadau katika kuchangisha fedha mitandaoni kwa ajili ya watoto wa rapa huyo, ambapo mchezaji maarufu wa zamani wa NFL, Reggie Bush alikuwa mmoja wa wachangishaji akilenga kupata $100,000, huku yeye binafsi akichangia $10,000.
Hata hivyo, baada ya familia hiyo kutoa tangazo rasmi, Bush aliondoa link hiyo kwenye mtandao na wadau wengine walifanya hivyo pia.
Nipsey alikuwa mchumi anayetunza fedha zake na kuwekeza kwenye mambo muhimu. Alifanikiwa kuwa na lebo yake, kufungua duka kubwa la nguo la Marathon pamoja na kumiliki eneo kubwa lenye majumba ya kupangisha.
Kwa mujibu wa TMZ, ingawa familia hiyo imewashukuru wadau hao kwa jinsi walivyoonesha kujali, imeeleza kuwa hata Nipsey Hussle mwenyewe angekuwepo asingependa kuona wanae wanachangiwa kwa jinsi alivyowawekea misingi bora ya kiuchumi.