Borussia Dortmund watakutana na Eintracht Frankfurt kwenye mchezo wa fainali wa kuwania ubingwa wa kombe la Ujerumani (DFB Pokal).
Borussia Dortmund wamepata nafasi hiyo kufuatia ushindi wa mabao 3-2 walioupata dhidi ya mabingwa wa soka nchini Ujerumani, FC Bayern Munich katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa usiku wa kuamkia leo mjini Munich kwenye uwanja wa Allianz Arena.
Marco Reus alitangulia kuifungia Borussia Dortmund dakika ya 19 akitumia vyema makosa ya Javi Martinez aliyerudisha mpira nyuma bila kuangalia hatari ya mpinzani.
Dakika ya 28 Javi Martinez alisawazisha makosa yake kwa kuifungia FC Bayern Munich bao la kusawazisha kabla ya Mats Hummels kuongeza bao la pili katika dakika ya 41.
Kipindi cha pili kilikuwa kizuri zaidi kwa Borussia Dortmund kwani waliweza kuwabana vyema wenyeji wao Bayern Munich na kufanikiwa kupata mabao mawili ya dakika za 69 na 74 kupitia kwa Pierre-Emerick Aubameyang na Ousmane Dembele.
Mchezo mwingine wa nusu fainali Eintracht Frankfurt ambao wanashika nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi ya Ujerumani (Bundesliga), walifanikiwa kutinga fainali baada ya kuifunga Borussia Monchengladbach kwa penati 7-6.
Mchezo wa fainali utachezwa Mei 27 katika dimba la Olympiastadion mjini Berlin.