Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Mayele amechimba mkwara mzito kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger kesho Jumapili (Mei 28) kwa kusema anaamini Young Africans ina nafasi kubwa ya kushinda ubingwa huo.
Young Africans itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kabla ya kwenda Algeria kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Juni 03.
Mayele kwenye mashindano hayo ndiye kinara wa ufungaji akiwa ameweka kambani mabao sita sawa na mshambuliaji wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro.
Nyota huyo ameongeza kuwa hatawaacha wapinzani wake hao kwa kuwa anataka kufunga bao dhidi yao na kuibuka kinara wa ufungaji bora katika Michuano hiyo msimu huu 2022/23.
Mayele amesema: “Tunafahamu huu ni mchezo ugumu kwa kuwa ni fainali na tunacheza dhidi ya timu ngumu na ni mara ya kwanza kwetu kufikia hatua hii kama mchezaji binafsi nina jukumu kubwa la kuisaidia timu kushinda ubingwa huu.
“Tumekamilisha maandalizi yetu na tupo tayari kuhakikisha tunashinda ubingwa, tunajua huu ni mchezo wenye presha kubwa lakini tupo hapa kuipigania nchi kushinda na nitafurahi nikifunga bao.”