Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amewataka mabeki wake kutofanya makosa  yasiyokuwa na ulazima nje ya 18 yatakayosababisha mipira ya adhabu golini kwao dhidi ya USM Alger ya nchini Algeria.

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa kesho Jumapili (Mei 28) saa 10 kamili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar. Mchezo wa pili utakuwa Algeria Juni 3.

Safu ya ulinzi ya Young Africans inaongozwa na nahodha Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Djuma Shaban na Kibwana Shomari ambao wamekuwa wakianza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.

Nabi amesema anakwenda kucheza dhidi ya USM Alger akiwa anaifahamu vizuri kimbinu, wakitumia mipira ya kutenga kupata mabao faulo na kona.

Nabi amesema kuwa tayari amewaandaa mabeki hao ili kuhakikisha wapinzani wao hawapati faulo za nje ya 18 huku wakipunguza mipira ya kona ambayo ni hatari kwa USM Alger kuicheza kwa vichwa.

Mtunisia huyo amesema kuwa kingine amewataka mabeki wa pembeni kutoruhusu mipira ya krosi kupigwa golini kwao, kwa lengo la kutowapa nafasi ya kucheza mipira ya juu huku akiamini mbinu alizowapa kwa siku hizi tatu kambini Avic Town, Kigamboni kuwaandaa.

“Maandalizi hayo niliyoyafanya yanatosha kabisa kwetu kupata ushindi, mabeki wangu nimewaambia wawakabe kwa makini na tahadhari ya hali ya juu wapinzani wetu ambao ninaamini watatumia muda mwingi kupoteza dakika, kwani ndio mbinu zao wanazozitumia wakiwa ugenini.

“Pia nimewataka viungo wangu kutowapa nafasi viungo wa wapinzani kumiliki mpira kwa muda mrefu, kwani watataka wapoteza muda kwa kukaa mpira, hapa nyumbani tunahitaji ushindi  wa mabao mengi ili yawe faida tutakaporudiana.

Ameongeza kuwa pia amewataka viungo wake wakabaji Mudathir Yahya na Yannick Bangala kutowapa nafasi ya kumiliki mpira viungo wa USM Alger ambao wameonekana wenye kasi na uharaka wa kupiga pasi zenye madhara golini kwao.

“USM Alger ni wazuri katika mipira ya ya kutenga, kwa maana ya faulo na kona hilo nimeshawaambia wachezaji wangu na kuwapa mbinu za uchezaji zitakazozuia mipango yao ya ushindi kwa kuanzia hapa nyumbani kabla ya kwenda kurudiana kwao.

“Katika mchezo huu tutamkosa Khalid Aucho, ni pengo lakini sio kubwa ninao wachezaji wengine uwezo wa kucheza na pengo lake kutoonekana akiwemo Bangala, Mudathiri na Mauya (Zawadi),” amesema Nabi.

Fiston Mayele: Nitapambana hadi niwafunge USMA
Rais Samia ataka uzingatiaji kiapo cha uaminifu, utunzaji siri