Kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama, amefichua moja ya sababu iliyopelekea Wekundu wa Msimbazi kufanya vibaya msimu huu ni kutokuwa na kikosi kipana na kupelekea wachezaji waliopo kucheza mechi mfululizo na hivyo kupata uchovu.

Akizungumza jijini, Dar es Salaam kuhusu tathmini ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2022/23 kwenye klabu yake ya Simba, Chama, alisema hawakuwa na msimu mzuri kutokana na kukosa kiwango kilichosimama, na badala yake wamekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka.

“Msimu, huu kuna mambo mengi kwetu yametokea, haukuwa msimu mzuri, kuna wakati tuko vizuri, wakati tunapambana hatupati matokeo mazuri, muda mwingine hapo chini hatuchezi vizuri, tulianza na Ngao ya Jamii tukapoteza, tukaanza ligi vizuri, baada ya hapo tukatapa droo na KMC na hadi tumefika hapa, kwangu mimi msimu ulikuwa mzuri kwa wengine.

Kuna mechi tulitakiwa tushinde ili tuwe kwenye nafasi nzuri, lakini tukatoka sare na kupoteza, ufinyu wa kikosi umetufanya tuwe na msimu mbaya au tuseme mgumu kwa sababu tukifanya mabadiliko ya kikosi tunaonekana,tumezidiwa kidogo na wapinzani, lakini nadhani ni suala la muda tu na mambo madogo madogo haya, yatakaa sawa,” alisema Chama.

Aliongeza pia mabadiliko ya makocha, wachezaji na mfumo nayo yalichangia kutofanya vyema, lakini kwa sasa kila kitu kimekaa sawa kocha yupo na wachezaji wameshaushika mfumo huku wakitarajia kuongeza nyota wapya watakaoongeza nguvu katika kikosi.

“Tunatakiwa tujipange, tujifunze tuanze vizuri msimu ujao, mimi kwangu naamini tuanzie upande wa viongozi, wameshaona matokeo ya msimu huu na wameshaona makosa, tuje kwetu wachezaji kila mmoja aangalie ni nini ambacho amekichagia kwenye timu, kikubwa au kidogo, na vile vizuri tuendelee navyo kwa msimu ujao,” alisema Chama.

Mzambia huyo aliwashukuru wanachama na mashabiki wa Simba kwa kuwaunga mkono vipindi vyote vya shida na raha na hata msimu huu ambao hawakufanya hawakuwaacha. Simba SC imepoteza vikombe vyote msimu huu na furaha yao pekee ni kuifunga Yanga mabao 2-0 katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara.

Akinamama waililia Serikali usaidizi kujikwamua kiuchumi
TMA yataarifu mwelekeo msimu wa kipupwe nchini