Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele, amesema kwa namna pekee itakayomfanya afanikishe malengo ya kutwaa Tuzo ya Ufungaji Bora ya Ligi Kuu Bara msimu huu ni kuongeza juhudi kwenye kutimiza majukumu ya timu.
Nyota huyo kwenye orodha ya watupiaji ni namba moja akiwa na mabao 15 na pasi moja ya bao, anayemfuatia ni Moses Phiri na Saidi Ntibazokiza ‘Saido’ wote wa Simba wametupia mabao 10 kila mmoja.
Mayele amesema, wanatambua kazi kubwa ipo kwenye michezo ambayo wanacheza kutokana na kila timu kupambana kusaka ushindi.
“Kwenye michezo ambayo tunacheza kila timu inahitaji ushindi, lakini kwa namna ambavyo tunashirikiana inaongeza nguvu kwenye upande wa kufanikisha malengo yetu.”
“Ikiwa timu itashinda kwanza hilo ni jambo la msingi, kasha kuhusu kutwaa Tuzo ya Ufungaji Bora litafuata, kikubwa ni malengo ya timu ambayo inahitaji ushindi,” amesema Mayele.
Young Africans ipo nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na alama 65 baada ya kucheza michezo 24, imefunga mabao 45.