Rais wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid Florentino Perez, amewataka wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo kumuachia suala la usajili wa kiungo kutoka nchini Hispania na klabu ya Man City Brahim Abdelkader Díaz.
Perez aliomba kuachia suala la usajili wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21, huku akiamini ataweza kummudu katika ushawishi wa kumtaka arejee nyumbani na kuitumikia klabu nguli ya Real Madrid.
Kiongozi huyo anatarajia kutumia nafasi ya Brahim kukataa kusaini mkataba mpya, huku mkataba wake na Man City ukisaliwa na muda wa miezi sita kabla ya kufikia kikomo, hali amabyo inatoa nafasi ya kufanya mazungumzo na klabu nyingine.
Hata hivyo imeelezwa kuwa Perez ataanza kuwashawishi wazazi wa kinda huyo ili kuangalia uwezekano wa kukamilisha ahadi aliyoitoa kwenye kikao cha bodi ya wakurugenzi wa Real Madrid, ambao mara kadhaa wamekua wakijadili uwezekano wa usajili wa mchezaji huyo ambaye anaitumikia timu ya taifa ya Hispania chini ya umri wa miaka 21.
Endapo mambo yatakwenda kama Parez anavyotarajia, huenda Real Madrid wakafaidika na usajili wa kiungo huyo mwezi June 2019, ambapo atakuwa mchezaji huru kuondoka Man City.
Brahimi alisajiliwa na Man City mwaka 2016 akitokea Malaga ya Hispania, na mpaka sasa ameshacheza michezo mitano chini ya utawala wa meneja Pep Guardiola.