Kundi la mataifa saba yanayoongoza kiuchumi limetaka wanajeshi wote wa Eritrea waliopo Kaskazini mwa Ethiopia kuondoka, huku taasisi ya kimataifa ya kufuatilia migogoro (ICG), ikionya dhidi ya kuendelea kwa mkwamo.
Taarifa ya pamoja ya Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa kundi la G7 iliyotolewa Ijumaa Aprili 2, imesema mchakato wa kuwaondoa wanajeshi hao lazima ufanyike kwa haraka.
“Tumelipokea tangazo la hivi karibuni la Waziri Mkuu Abiy Ahmed (wa Ethiopia) kwamba wanajeshi wa Eritrea wataondoka kutoka jimbo la Tigray. Mchakato huo lazima uwe wa haraka, usio masharti na unaoweza kuthibitishwa (kwamba unafanyika),” limesema tamko hilo lililotolewa mjini Berlin, Ujerumani.
Kiongozi wa muda wa jimbo hilo, Mulu Nega, amesema suala la kuondoka kwa wanajeshi hao wa Eritrea ni mchakato ambao hauwezi kukamilika haraka.
Wakizungumza na Shirikala habari la AFP, wakazi wa miji kadhaa ya Tigray wamesema hata baada ya kutolewa tangazo hilo la Waziri Mkuu Abiy, wanajeshi wa Eritrea wamezidi kujiimarisha kwenye baadhi ya maeneo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, mashahidi waliripoti kuyaona magari manne yakiwa yamejaa wanajeshi wa Eritrea yakiwasili kwenye mji wa Edaga Hamus.
Awali, serikali za Ethiopia na Eritrea zilikuwa zikikanusha kuwepo kwa wanajeshi wa Eritrea katika jimbo la Tigray, zikipingana na ushahidi unaotolewa na wakazi wa huko, makundi ya haki za binadamu, wanadiplomasia na hata baadhi ya raia na maafisa wa kijeshi wa Ethiopia.
Abiy Ahmed, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na Waziri Mkuu wa Ethiopia, alituma wanajeshi kwenye jimbo hilo la Kaskazini mwa nchi yake mwezi Novemba 2020 kwa lengo la kuwatia nguvuni na kuwanyang’anya silaha viongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF), ambacho kiliwahi kulitawala jimbo hilo na Ethiopia nzima.
Wakati huo, Abiy alisema hatua iliyo ilikusudiwa kujibu uchokozi uliofanywa na TPLF kwa kuzishambulia kambi za jeshi la serikali ya shirikisho.
Ikiwa ni takribani miezi mitano tangu silaha ya kwanza risasi ya kwanza kusikika katika jimbo hilo, kundi la ICG katika ripoti yake lilioichapisha leo Ijumaa Aprili 2, limeripoti kuwa ukandamizaji umekuwa ukiendelea kwenye maeneo ya kati na kusini mwa Tigray, licha ya Abiy kutangaza ushindi kwenye operesheni hiyo wiki chache baada ya kuanza.
Mashirika ya haki za binaadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch, yanavituhumu vikosi vya Eritrea kwa mauaji ya kimbari dhidi ya mamia ya watu kwenye mji wa Axum jimboni Tigray, yaliyotokea mwezi Novemba, huku shirika la habari la AFP likiripoti kuhusu mauaji mengine ya kimbari yaliyofanywa na wanajeshi hao wa Eritrea kwenye mji wa Dengolat.