Beki wa kati kutoka nchini Brazil na Klabu ya Arsenal Gabriel Magalhaes ameonesha kuwa na mapenzi ya dhati na klabu hiyo ya jijini London, ambayo inaendelea kujitetea katika mbio za ubingwa wa England msimu huu 2022/23.
Arsenal ilififisha matumaini ya Ubingwa juzi Jumatano (April 26) baada ya kufungwa 4-1 na Manchester City iliyokuwa nyumbani katika Uwanja wa Etihad mjini Manchester.
Gabriel ambaye amekuwa beki wa kutumainiwa tangu aliposajiliwa Arsenal msimu wa 2020/21 akitokea Lille ya Ufaransa, amesema anaipenda sana The Gunners na dhamira yake ni kuhakikisha wanatwaa mataji akiwa na klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London.
“Naipenda klabu hii, napenda kikosi hiki na ninapenda kuwa hapa na kutimiza ndoto zangu nikiwa hapa Arsenal”
“Hatukati tamaa, tutaendelea kupambana ili kuipa heshima klabu hii na tutapambana hadi mwisho.” amesema Gabriel
Bado Arsenal inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa na alama 75, ikifuatiwa na Manchester City yenye alama 73, lakini bado ina mchezo mmoja mkononi.
Arsenal Jumanne (Mei 02) itacheza dhidi ya Chelsea huku Manchester City ikitarajiwa kupapatuana na Fulham Jumapili (Aprili 30).