Uongozi wa Geita Gold FC umetangaza vita ya kumbakisha Mshambuliaji George Mpole kwenye kikosi cha klabu hiyo, kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Geita Gold FC itashiriki kwa mara ya kwanza Michuano ya Kimataifa (Kombe la Shirikisho Barani Afrika), kufuatia kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita 2021/22.
Mwenyekiti wa Geita Gold Costantine Morandi amesema, wapo kwenye mchakato mzito wa kuhakikisha Mpole anaendelea kubakia klabuni hapo, huku wakiamini atakua msaada mkubwa kwenye michuano ya Kimataifa.
Amesema wanatambua kuna mipago ya Mshambuliaji huyo kuwindwa na Klabu za Ligi Kuu kutoka na Uwezo waliouonesha msimu uliopita, hivyo wanaendelea kupambana.
“Tupo kwenye mchakato wa kumbakisha Mpole hapa Geita Gold FC, tumepata ofa kadhaa hadi sasa, lakini tunapambana bila kuchoka kumshawishi mchezaji, ili aendelee kuwa nasi kwa msimu ujao,”
“Tunaamini Mpole atashawishika kubaki na sisi kwa msimu ujao, endapo mambo yatakua tofauti hatutakuwa na mpango mwingine, zaidi ya kumuachia, lakini kipaumbele ni kupambana kwanza ili abaki.” Amesema Costantine
Tayari Geita Gold inatajwa kumsajili kwa Mkopo Mshambuliaji kutoka Burkina Faso na klabu ya Young Africans Yacouba Sogne.