Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Gamondi amesema haikuwa rahisi kwao kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuweka Rekodi ya kutinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza.
Juzi Jumamosi (Februari 24) Young Africans ilifuzu Robo Fainali kwa kishindo kwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikiwa na alama nane na kuungana na Al Ahly ambao wanaongoza msimamo wa Kundi D wakiwa na alama tisa.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema ulikuwa mchezo mgumu, lakini hana budi kumshukuru Mungu na wach4ezaji wake kwa kazi nzuri, ambayo imewapa ushindi mkubwa wa mabao 4-0, na kutinga robo Fainali ya michuano hiyo baada ya miaka 25.
“Hatua ya makundi hatukuanza vizuri kwa kuwa tulikuwa kwenye kundi gumu, lakini tumepambana ya kutofuzu, naamini kuna baadhi ya watu hawakuamini kamna tunaweza kufika hapa.
“Kuna watu walikuwa na furaha baada ya kupoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya Makundi, lakini sisi kama Young Africans hatukukata tamaa tulipambana hadi hapa tulipofuzu,” amesema Gamondi.
Naye Kocha Mkuu wa CR Belouizdad, Marcos Paqueta kabla ya kuondoka nchini amesema ilikuwa ngumu kwao kucheza mechi kwenye hali ya hewa ya joto namna ile, ilikuwa kikwazo kwao kupata ushindi ndio maana wamepoteza kwa idadi kubwa ya mabao.
“Baada ya bao la kwanza tulijaribu kusawazisha tukafanya makosa ambayo yakaendelea kuwapa faida wapinzani wetu ambao walinufaika na kupata mabao mengine matatu na kutupotezea malengo yetu hivyo tunajipanga na mchezo wa mwisho,” amesema Paqueta.