Gavana wa Migori nchini Kenya, Okoth Obado anayetuhumiwa kushiriki mauaji ya mpenzi wake ataendelea kusota ndani ya selo za polisi baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi lake la dhamana.
Obado na wenzake wawili ambao ni Michael Oyamo na Caspal Obiero watakaa selo kwa siku nyingine 12, hadi Oktoba 8 mwaka huu ambapo maombi yao ya dhamana yatakapoanza kusikilizwa upya.
Watatu hao wanashtakiwa kwa kosa la kumteka na kumuua kikatili mwanafunzi wa kike wa chuo kikuu, Sharon Otieno, aliyekutwa akiwa ametupwa msituni magharibi kwa Kenya.
Ripoti ya uchunguzi wa daktari inaonesha kuwa Sharon aliyekuwa mjamzito alibakwa na kuchomwa visu mara nane katika maeneo ya shingoni, tumboni na mgongoni hadi kufa.
Sharon alikuwa na uhusiano wa mapenzi na Gavana Obado ambaye ni mwanandoa.
Washtakiwa wengine walikuwa na uhusiano wa karibu na Gavana huyo; Oyamo akiwa ni msaidizi wake, na Obiero akiwa ni katibu wa kaunti hiyo.
Watuhumiwa wote wamekanusha kuhusika na tukio hilo.