Faisary Ahmed – Kagera.
Katika kufikia lengo la kuhakikisha kila mtoto anasajiliwa ifikapo mwaka 2025, Viongozi wa Mkoa wa Kagera wamehimizwa kutoa elimu na hamasa kwa kushirikiana na wazazi kujitokeza kuwasajili watoto wao, ili waweze kupata vyeti vya kuzaliwa hali itakayosaidia kutambuliwa na taarifa zao kuingizwa katika mfumo rasmi wa utambuzi wa serikali.
Hayo yamezungumzwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Paulini Gekul wakati wa uzinduzi wa mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano Mkoani Kagera, huku zaidi ya watoto milioni 8 wakiwa wamesajiliwa hadi sasa nchini.
Amesema, “nitoe rai kwenu wakurugenzi, madiwani na viongozi wa mitaa kuhakikisha kwamba kazi hii inapoendelea kwenye wilaya zenu taarifa ziwafikie wananchi na itapendeza kama matangazo yatatolewa kwa wakati kwani Mwananchi akikosa taarifa hii wadau wetu wakiondoka kuelekea mkoa mwingine atajisikia vibaya.”
Aidha Gekul meongeza kuwa, “wakati tunaendelea kusajili watoto chini ya miaka mitano pale ambapo wananchi wanahitaji ufafanuzi wa jinsi gani akiwa mtu mzima apate cheti hiki basi RITA, mwenyekiti wa bodi na timu yako msisite kutoa elimu hii kuhakikisha kwamba yeyote Mtanzania anayetaka cheti anapata lakini pia viwango vile viwe wazi.”
Naye Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amehaidi kuwa zoezi hilo litasimamiwa kikamilifu na kutoa wito kwa wasajili na wazazi kuwa makini kwenye kuandikisha majina ya watoto hao.
Amesema, “tumejizatiti kusimamia mpango huu kikamilifu ili kuhakikisha kwamba watoto wote wanaostahili kupata huduma hii wanaipata bila kikwazo chochote na pia nitoe wito zoezi hili likiwa linafanyika usahihi wa majina uangaliwe vizuri ili mtoto anaposajiliwa majina yake yawe sahihi ili baadae akiendelea kutumia majina hayo yaendelee kuwa sahihi katika vyeti vinavyofata.”
Kwa upande wake Mbunge wa Bukoba mjini, Steven Byabato na Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Christopher Paranjo wamebainisha changamoto inayokwamisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo ni kutokana kuwa mkoa huo kuwa eneo la mpakani na wameitaka RITA kushughulikia changamoto hiyo ili kusaidia wepesi wa zoezi hilo.
Wakizungumza kwa nyakatai tofauti, Wakazi wa Mkoa wa Kagera wamesema zoezi hilo limewasaidia kwa awali lilikuwa mwarobaini kwao kutokana na kutumia muda mwingi na mwendo mrefu kupata huduma ya vitambulisho vya Taifa.
Mkoa wa Kagera, ni miongoni mwa mikoa 24 ambayo imefikiwa na huduma hii ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano Tanzania Bara ambapo zaidi ya watoto laki 4 wanatarajia kusajiliwa huku mkoa wa Kigoma na Dar es Salaam imebakia kwa sasa kupata huduma hiyo.