Watendaji wa Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Fedha Nchini Nigeria (EFCC), wamewakamata washukiwa 140 wa ulaghai wa mtandao, maarufu kama yahoo boys.
Kupitia taarifa ya Tume hiyo iliyotolewa na Msemaji wake Wilson Uwujaren, imesema washukiwa wanne kati ya hao, waliachiwa huru baada ya kujiridhisha kuwa hawana hatia.
“Tumewakamata watu 140 na wengi ni Vijana wadogo, hawa ni maarufu kwa makosa ya kimtandao na wanafahamika kama yahoo boys,” alisema Uwujaren.
Watu hao ambao wengi wao wana umri kati ya miaka 16 – 40, walikamatwa kwenye mazingira tofauti ya Hotel maarufu Nchini humo za Lakers Lounge & Bar na De Butlers, zilizopo Ikorodu Jimbo la Lagos.
Inadaiwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao, kulitokana na taarifa za kijasusi za kuhusika kwao katika ulaghai unaohusiana na mambo ya kimtandao, ikiwemo kuwaibia watu fedha.
Shirika hilo la kupambana na ufisadi, limesema washukiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
“Hii haikubaliki na tunaikemea vikali, wale wote wenye tabia kama hizi wanatakiwa kuziacha mara moja kabla sheria haijawakuta na watuhumiwa hawa tunawapeleka Mahakamani haraka,” alisisitiza Msemaji wa EFCC, Uwujaren.
Bidhaa zilizopatikana kutoka kwa washukiwa hao ni pamoja na magari ya kigeni, vifaa vya kielektroniki, kompyuta ndogo na simu za rununu.