Serikali imesema imekuwa ikitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wanaougua maradhi yasiyoambukiza, ambao wamethibitika kutokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu yao.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Chaani, Juma Hamad aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa matibabu bure kwa maradhi yasiyoambukiza kama Kisukari, Presha na Shinikizo la Damu.

“Serikali imekuwa ikitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyoambukiza, haya nia yale magonjwa ambayo yamethibitika kuwa hayana uwezo wa kugharamiwa,” alifafanua Dkt. Mollel.

Amesema, Serikali ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa muswada wa Bima ya afya kwa wote, ambao utawezesha wananchi kupata tiba katika vituo vyote vya huduma za afya nchini.

Akijibu Swali la nyongeza la mbunge huyo aliyehoji usumbufu wanaopata wazee hospitalini wakati wa kupata huduma, Dkt. Mollel amewasisitiza wataalam kufuata maagizo yanayotolewa na Viongozi na kuhakikisha Wazee wanapata matibabu bure katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

“Agizo kwa Waganga wote wa Mikoa na Wilaya, suala la matibabu kwa wazee ni bure na wanatakiwa kuwa na dirisha lao la kupata huduma, hatutegemei kusikia tena malalamiko ya wazee,” ameagiza Naibu Waziri wa Afya.

Suala la wazee kulalamika juu ya kukosa huduma za bure kama sera za Wizara ya Afya zinavyoelekeza, limekuwa likitukia katika baadhi ya Vituo vya kutolea huduma za Afya nchini, hali ambayo inayoleta mkanganyiko kwa Wananchi.

Simba SC yapangua hoja ya Chama kuvunja mkataba
Senzo: Tuna ofa mbili za Fiston Mayele