Kesi inayomkabdili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake sita inatarajiwa kusomewa hukumu hii leo Juni 10, 2022.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021, ilikuwa isomwe Mei 31, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha Fadhili Mbelwa lakini iliahirishwa kwa sababu zilizotajwa kuwa ni kutokuwepo kwa Hakimu Patricia Kisinda aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo.

Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka jana na kusomewa mashitaka matano.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Octoba mwaka jana ambao upande wa Jamhuri uliongozwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Felix Kwetukia akisaidiwa na wenzake wanne na walisikilizwa mashahidi 13 wakiwa na vielelezo 9 na upande wa utetezi ulipeleka mashahidi wanne.

Upande wa utetezi uliongozwa na Wakili Mosses Mahuna akisaidiwa na wenzake wanne na katika shitaka la kwanza walishtakiwa wote ambapo Sabaya alitajwa kuhusika kutumia vibaya madaraka yake akiwa mtumishi wa umma kwa kutumia genge lake la uhalifu.

Shitaka la pili Sabaya alishtakiwa peke yake kwa kuwa mtumishi wa umma na kushawishi rushwa ya shillingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara maarufu jijini humo, Francis Mrosso ili amsaidie kumvusha katika kesi ya ukwepaji kodi iliyokuwa ikimkabili na shitaka la tatu ni kuomba rushwa kwa mfanyabiashara huyo.

Shitaka la nne ni kutakatisha fedha haramu lililokuwa likiwakabili washitakiwa 7 ambapo walidaiwa kuchukua fedha za Mrosso na kuzitumia katika matumizi yasiyo sahihi.

Shitaka la tano linalomkabili Sabaya ni matumizi mabaya ya madaraka ambapo kwa nyakati tofauti alitenda makosa kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

Mei 6, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilimuachia huru Sabaya na wenzake wawili waliokua wamekata rufaa ya kupinga kuhukumiwa miaka 30 kwenda jela kila mmoja baada ya Hakimu kubaini kuwa kulikuwa na mapungufu katika mwenendo mzima  kesi, pamoja na kutofautiana na mashahidi lakini alisema Sabaya ataendelea kukaa mahabusu kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Mahakama yafuta kesi ya Makonda
Genge la uhalifu 'yahoo boys' mikononi mwa polisi