Mshambuliaji George Mpole amesema bado hajafahamu wapi atakapocheza soka lake msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Mpole aliyeibuka Mfungaji Bora msimu uliopita, ametoboa siri hiyo baada ya jina lake kusitishwa kutajwa katika usajili wa klabu za Simba SC, Young Africans na Azam FC, ambazo zilitajwa kuwa kwenye mbio za kumuwania kabla ya msimu wa 2021/22 haujamalizika.
Mshambuliaji huyo amesema kwa sasa yupo Mbeya akiendelea na Maisha ya likizo fupi huku akifanya mazoezi binafsi, lakini ukweli ni kwamba hana uhakika wapi atakapocheza msimu ujao wa 2022/23.
Hata Hivyo Mpole amesema anatamani kucheza katika timu ambayo itampa kipaumbele cha kutumika kwenye kikosi ch kwanza, ili kuendeleza moto aliouwasha msimu wa 2021/22, kwa kupachika mabao 17.
“Nipo Mbeya ninaendelea na Maisha yangu ya likizo fupi, ninafanya mazoezi yangu binafsi, sijafahamu wapi nitakapocheza msimu ujao hadi sasa, binafsi sihitaji kulizungumza hilo kwa sababu wapo wakuu wangu ambao wana mamlaka na hilo,”
“Nahitaji kucheza katika timu ambayo itanipa kipaumbele cha kucheza katika kikosi cha kwanza ili niweze kuendeleza pale nilipoishia, haitakua sawa kwenda sehemu ambayo nitakaa benchi, kwani wadau wanatamani kuona muendelezo wangu mzuri baada ya nilichokifanya msimu ulioisha.” Amesema Mpole