Mlinda mlango mkongwe kutoka nchini Italia, Gianluigi Buffon amewatoa hofu baadhi ya wadau wa soka duniano akieleza kuwa hatua ya kusajiliwa na klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain akitokea Juventus, haimaanishi kuwa atakua chaguo la kwanza.
Buffon ameweka wazi suala hilo kufuatia minong’ono iliyozuka baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Arsenal uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita nchini Singapore, ambapo PSG walikubali kibano cha mabao matano kwa moja.
Katika mchezo huo Buffon alikubali kufungwa mabao matatu, kabla ya kumpisha Kevin Trapp aliyefungwa mengine mawili.
Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 40, amesema hatua ya kusajiliwa kwake klabuni hapo ni sawa na inavyokua kwa wachezaji wengine na kwamba hatma ya kucheza ama kutokucheza kwenye kikosi cha kwanza inakua mikononi mwa meneja/kocha.
“Sijahakikishiwa na mtu yoyote kama nitakua chaguo la kwanza, nimesajiliwa kwa mipango ya meneja na ninaamini nipo hapa kuwania nafasi dhidi ya wachezaji wenzangu, ili tufanikishe lengo la PSG kwa msimu ujao,” Buffon anakaririwa.
“Nilipokua na miaka 24 niliwahi kuambiwa na mmoja wa wakufunzi wangu, nisijiamini kupita kiasi na haitatokea kuwa chaguo la kwanza milele. Aliniusia kutegemea ushindani kwani vipaji vya soka hupanda na kushuka,” aliongeza.
Buffon ana kazi nzito ya kuhakikisha ana kuwa na kiwango maridhawa na kuwapiku washindani wake katika lango la PSG Alphonse Areola na Kevin Trapp aliowakuta klabuni hapo.
Usajili wa mkongwe huyo ulipewa uzito na meneja mpya wa PSG, Thomas Tuchel ambaye alihitaji mlinda mlango mwenye uzofu na ambaye ataweza kutoa changamoto kwa walinda milango aliowakuta klabuni hapo.