Kauli ya Rais wa kwanza wa Zimbabwe, Robert Mugabe aliyoitoa jana kuwa hatampigia kura Rais Emmerson Mnangagwa kwenye uchaguzi unaoendelea leo nchini humo, imesababisha kunyang’anywa wanajeshi waliokuwa wanalinda nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa msemaji wa chama cha National Patriotic Front (NPF) ambacho Mugabe alionesha kukiunga mkono, Jealousy Mawarire hatua hiyo ilichukuliwa punde mwanasiasa huyo mkongwe alipomaliza kuzungumza na waandishi wa habari.

Mawarire ameeleza kupitia Twitter kuwa wanajeshi tisa waliokuwa wanalinda makazi ya Mugabe, maarufu kama The Blue House/Roof, sio tu kwamba waliondolewa bali pia waliharibu sehemu ya makazi hayo.

Hata hivyo, wakosoaji wa Mugabe wanadai kuwa uamuzi wa kuondolewa kwa wanajeshi hao kunatokana na kauli yake kuwa amewekwa katika kifungo cha nyumbani na sio kwamba analindwa.

Jana, Mugabe alizungumza na vyombo vya habari kuhusu msimamo wake kisiasa na akaweka wazi kuwa hatampigia kura Mnangagwa kwa madai kuwa alifanya njama ya mapinduzi ya kijeshi kumuondoa madarakani mwaka jana.

Mnangagwa aliyekuwa Makamu wa Mugabe na mtu wake wa karibu tangu nchi hiyo ilipopata uhuru, leo anawania nafasi hiyo baada ya kipindi cha mpito kumalizika.

Anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Nelson Chamisa ambaye ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change Alliance. Kura za awali za utafiti zilimpa Chamisa 37%, ikiwa ni alama 3 tu nyuma ya Mnangagwa.

Tayari Mugabe ameshapiga kura yake akiungana na mamilioni ya wananchi waliojitokeza kwenye vituo vya kupigia kura. Ingawa kura ni siri, tayari kura ya Mugabe inaeleweka kuwa haikumchagua mgombea wa chama alichokiasisi cha Zanu-PF.

Ndugai anena kuhusu Waitara, sasa kuiandikia barua NEC
Gianluigi Buffon aahidi kupambana PSG