Hatua ya kurejea kwa Kiungo Mshambuliaji kutoka Zambia Clatous Chama kwenye kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, imemfurahisha Kocha Mkuu wa klabu hiyo Didier Gomes.
Chama alikua mapumziko nchini kwao Zambia, baada ya kufiwa na Mkewe mwanzoni mwa mwezi huu, na kwa mara ya kwanza alirejea kikosini Juzi Jumanne (Juni 22), kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Katika mchezo huo kiungo huyo alifunga bao la nne na la ushindi kwa Simba SC, huku mabao mengine yakifungwa na John Bocco, Rally Bwalya na Luis Miquissone.
Kocha Gomes amesema: “Nimefurahishwa na kiwango alichokionesha ingawa ameripoti juzi mazoezini akitokea Zambia, lakini amecheza vizuri na tulipanga kumpa dakika 30 kwa ajili ya kumrudisha mchezoni ili kwenye mchezo wetu dhidi ya Young Africans awe ni miongoni mwa wachezaji watakaoanza,”
Baada ya kuifunga Mbeya City FC mabao 4-1, Juzi Jumanne (Juni 22) Simba SC imefikisha alama 73 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiiacha Young Africans yenye alama 67 zinazoiweka nafasi ya pili huku Azam FC wakiwa nafasi ya nne kwa kumiliki alama 64.
Kwa sasa Simba SC inajiandaa na mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), utakaochezwa mjini Songea mkoani Ruvuma dhidi ya Azam FC, Jumamosi (Juni 26) Uwanja wa Majimaji.
Mchezo mwingine wa Nusu Fainali ya michuano hiyo utachezwa kesho Ijumaa (Juni 25) mjini Tabora kati ya Young Africans dhidi ya Biashara United Mara, Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi.