Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes amesema baada ya kucheza michezo miwili ya Ligi Kuu msimu huu 2021/22, amejifunza jambo ambalo litakisaidia kikosi chake kwenye michezo inayofuata.
Gomes alishuhudia kikosi chake kikianza kwa sare ya 0-0 dhidi ya Biashara United Mara, kisha kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC mjini Dodoma.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema wakati wanaanza msimu ugenini wachezaji wake walikua hawafahamu ugumu na changamoto za ushindani wa Ligi Kuu msimu huu, na ndio maana mambo yalionekana kuwa magumu kwao.
Amesema kwa kutambua hilo, wachezaji wake wamefahamu namna ya kupamba dhidi ya timu shiriki za Ligi Kuu msimu huu, hivyo watakaporejea baada ya kupisha mapumziko ya michuano ya kimataifa watakua na utofauti mkubwa.
“Tulianza kwa shida msimu huu kwa kuwa hatukujua ligi inakwendaje na hilo limetufanya tuweze kujua namna gani tunaweza kwenda hiloawali lilitufanya tukashindwa kupata ushindi mchezo wetu wa kwanza mbele ya Biashara United.
“Kwa sasa tumejua aina ya ligi ilivyo na mtindo ambao unahitajika tutakwenda sawa na imani yetu ni kuona kwamba tunapata matokeo chanya kwenye mechi zetu ambazo tutacheza,” amesema kocha Gomes.
Simba SC inamiliki alama 4 zinazoiweka katika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22, baada ya kucheza michezo miwili dhidi ya Biashara United Mara na Dodoma Jiji FC.