Kipigo cha jana cha 2-1 dhidi ya Newcastle kimemnyong’onyeza kocha wa Manchester City, Pep Guardiola na kupunguza matumaini ya kuwa kinara wa Ligi Kuu ya Uingereza.
Kipigo cha jana kimewapa nafasi zaidi Liverpool kuendelea kujichimbia kileleni, ikifukuzia kuweka tofauti ya alama saba muhimu dhidi ya Manchester City inayowanyemelea.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi ya jana, Guardiola alisema kuwa ni muhimu kukubaliana na matokeo ya mpira wa miguu kwakuwa ni ushindani na kwamba unaweza kushindwa. Alikiri kuwa kutokana na matokeo yao, kikosi chake kina mlima mrefu mbele yao kuifikia Liverpool.
“Ni ngumu sana. Tuna nafasi, hatuna faida ya wazi ya kupata ushindi lakini tunapaswa kuendelea. Tunapaswa kucheza michezo yetu na kufahamu tunachotakiwa kufanya,” alisema Guardiola.
“Tulikuwa na nafasi leo kupunguza tofauti ya alama za anayeongoza. Kesho kuna mechi ya mshindani wetu. Unapokuwa nyuma unapaswa kushinda mechi zako, lakini hatukufanya hivyo,” aliongeza.
Hata hivyo, kocha huyo hakutaka kuwatupia mzigo wa lawama wachezaji wake, badala yake aliamua kukumbushia jinsi ambavyo wamekuwa wakifanikiwa.
Leo, Liverpool itamenyana na Leicester City ambayo inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi, na wengi wanaipa nafasi klabu hiyo ya Anfield kujipatia ushindi na kumuongezea tabasamu meneja Jürgen Klopp.